Umewahi kujiuliza fisi anatamani maisha gani? Je, angependa kuishi akiwa amefungwa kwa minyororo ndani ya makazi ya binadamu? Je, anafurahia kutembelezwa mitaani kwa ajili ya burudani? Au kama angepewa nafasi ya kuchagua, angekimbilia porini, ambako ndiko nyumbani kwake?
Maswali haya yameibuka tena baada ya kurushwa kwa makala katika moja ya vituo vya televisheni nchini, ikionesha baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa ambako bado kuna mila za kufuga fisi kama sehemu ya urithi wa kitamaduni unaopitishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
Ni kweli, tamaduni ni sehemu muhimu ya utambulisho wetu. Zinabeba historia, maarifa na simulizi za mababu zetu. Lakini swali kubwa la kujiuliza ni hili: Je, kila tamaduni ya kale inapaswa kuendelea bila kuangalia athari zake kwa viumbe wengine?
Fisi ni mnyama wa porini. Ameumbwa kukimbia umbali mrefu kutafuta chakula, kuwasiliana na kundi lake na kuzunguka katika maeneo makubwa ya asili. Anapofungwa kwa minyororo au kuwekwa katika mazingira yasiyo ya asili yake, sehemu kubwa ya uhuru wake hupotea.
Pengine hatuoni maumivu yake kwa sababu hawezi kuzungumza lugha yetu. Hatusikii malalamiko yake wala kuona machozi yake. Lakini ukweli ni kwamba mnyama huyu, kama walivyo viumbe wengine, huhitaji nafasi, uhuru na mazingira yanayomruhusu kuishi maishaaliyoambiwa
Wataalamu wa uhifadhi wamekuwa wakisisitiza kuwa wanyamapori wana nafasi muhimu katika mifumo ya ikolojia. Fisi, ambaye mara nyingi huchukuliwa vibaya na baadhi ya watu, ni mmoja wa wasafishaji wakubwa wa mazingira ya porini. Hula mizoga na kusaidia kuzuia kuenea kwa magonjwa yanayoweza kusababishwa na mabaki ya wanyama waliokufa.
Tunapomtoa porini na kumweka kifungoni kwa ajili ya desturi au burudani, si tu kwamba tunamnyima uhuru wake, bali pia tunapunguza mchango wake katika mazingira ya asili.
Hii haimaanishi kuwa tunapaswa kuzipuuza tamaduni zetu. La hasha. Badala yake, tunapaswa kutafuta namna ya kuzihifadhi kwa njia zinazokwenda sambamba na uelewa wa kisasa kuhusu ustawi wa wanyama na uhifadhi wa maliasili. Tunaweza kuenzi historia ya mila hizi kupitia simulizi, makumbusho, maonesho ya kitamaduni na elimu kwa vijana, bila kuwafanya wanyamapori kuwa wafungwa wa tamaduni hizo.
Kadiri tunavyozidi kuelewa hisia na mahitaji ya viumbe wengine, ndivyo tunavyozidi kuwa walinzi bora wa uumbaji. Fisi, kama walivyo tembo, simba na wanyamapori wengine, hawakuumbwa kwa ajili ya minyororo. Waliumbwa kwa ajili ya uhuru.
Labda wakati umefika wa kujiuliza tena: Je, tunataka kurithisha vizazi vijavyo kumbukumbu za fisi waliofungwa, au tunataka kurithisha Tanzania yenye wanyamapori walio huru katika mazingira yao ya asili?
