Mashabiki wa Grand Theft Auto (GTA) sasa wanasikilizia siku baada ya kampuni ya Rockstar Games kufungua rasmi pre-order za GTA VI na kuachia picha zaidi ya 60 zinazoonesha mandhari, wahusika na baadhi ya vipengele vipya vya game hio.
GTA VI ni miongoni mwa game inayosubiriwa zaidi duniani, inaachiwa rasmi Novemba 19, 2026 kwa watumiaji wa PlayStation 5 na Xbox Series X|S.
Rockstar imetangaza kuwa toleo la kawaida la mchezo huo litauzwa kwa Tshs. 220,000 huku toleo la Ultimate Edition likiuzwa kwa zaidi ya Tshs. 270,000.
GTA VI itawarejesha wachezaji maarufu wa Vice City, safari hii likiwa katika toleo la kisasa zaidi, huku simulizi kuu likiwahusu wahusika wawili, Jason na Lucia, ambao wameelezwa kuwa na mahusiano yanayofanana kama Bonnie na Clyde.
Miongoni mwa mambo mapya yatakayopatikana katika mchezo huo ni mfumo wa mitandao ya kijamii ndani ya mchezo, ambapo wachezaji wataweza kutazama video fupi, kufuatilia "influencers" na kugundua missions mpya kupitia matukio yanayotokea katika GTA.
Lakini jambo lililozua mjadala mkubwa mtandaoni ni uamuzi wa Rockstar kutotoa CD (hard copy), Badala yake, wateja watakaonunua nakala za dukani watapata boksi lenye code maalum ili kupakua game pekee.
Mashabiki wengi wamesema hatua hiyo itaua soko la kuuza au kukopeshana michezo, huku wengine wakihofia kuwa itawaathiri wachezaji wenye mtandao wa internet usio na kasi au wasio na mabando/WiFi ya uhakika.
Kwa wachezaji wa Afrika, hasa nchi ambazo hazina maduka rasmi ya PlayStation, mfumo huo unaweza pia kuleta changamoto za "region lock", ambapo code ya mchezo inaweza kushindwa kufanya kazi ikiwa haitalingana na akaunti ya mtumiaji.
Licha ya mjadala huo, wachambuzi wa sekta ya michezo ya video wanaamini GTA VI inaweza kuwa moja ya launching kubwa zaidi huku ikitarajiwa kuvunja rekodi za mauzo ndani ya siku chache baada ya kutolewa.
