Barabara mpya za Dar kuja na mifereji na taa za kisasa

 

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam unaendelea kutekeleza mradi wa DMDP Awamu ya Pili (DMDP II), unaohusisha ujenzi wa kilomita 250 za barabara katika wilaya zote tano za mkoa wa Dar es salaam.

Mhandisi Masatu Ndango ameeleza hayo kwa niaba ya Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Godfrey Mkinga, kuwa barabara hizo zinajengwa kwa kiwango cha lami na baadhi ya barabara kwa tabaka la zege ili kuboresha usafiri na kurahisisha shughuli za kiuchumi.

Alisema mradi huo unatekelezwa kwenye wilaya zote za mkoa wa Dar es salaam ikiwemo wilaya ya Ilala, Kinondoni, Ubungo, Temeke na Kigamboni.

"Lengo ni kuunganisha wananchi kwa urahisi zaidi, kupunguza changamoto za usafiri na kufungua fursa za biashara katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es salaam" alisema.

Kwa mujibu wa TARURA mkoa wa Dar es salaam, barabara hizo zinaambatana na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua pamoja na taa za barabarani ili kuongeza usalama na matumizi ya miundombinu hiyo wakati wote wa mchana na usiku.

Alisema baadhi ya barabara zinazotekelezwa zipo katika kata za ToaNgoma, Temeke, Chang'ombe, Mbagala, Keko, Yombo Vituka, Azimio na kata ya Miburani katika wilaya ya Temeke, na barabara zingine kwenye wilaya zingine zote za mkoa wa Dar es salaam

Mbali na ujenzi wa barabara mpya, mradi huo pia unahusisha maboresho ya maeneo yenye msongamano na changamoto za usafiri ili kurahisisha mawasiliano kati ya maeneo ya pembezoni na katikati ya jiji.

"Tunaishukuru serikali yetu chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwezesha bajeti, usimamizi na uwezeshaji wa miundombinu yote ya maendeleo. Mpaka sasa mradi huu unaenda kuleta maendeleo ya moja kwa moja kwa kila mtanzania." alisisitiza mhandisi.

Mhandisi Ndango alisema kuwa barabara hizo zinatarajiwa kuchochea biashara, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuongeza upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

"Miundombinu bora ina maana ya safari fupi, biashara zaidi na maisha bora kwa wananchi," alisema.

Mkoa wa Dar es Salaam una mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 5057.7 unaohudumiwa na TARURA kwa ajili ya kuimarisha huduma za usafiri na maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, alieleza kuwa mkoa unaendelea kufanya matengenezo ya kawaida, sehemu korofi na matengenezo maalum katika mtandao wote, na ujenzi wa madaraja pamoja na makalavati katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam.

Pia amemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe kwa kuendelea kutoa miongozo ya ujenzi na utekelezaji wa miradi yote ya TARURA ikiwemo katika mkoa wa Dar es salaam, kwa kushirikiana na uongozi wote wa mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam chini ya Mhe. Albert Chalamila