DIT: Wamiliki wa magari waongezeka kufunga mifumo ya gesi asilia


Na Charles Mkoka 

Dar es Salaam. Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imesema idadi ya wananchi wanaotaka kufunga mifumo ya gesi asilia kwenye magari imeongezeka kutokana na gharama za mafuta kuendelea kupanda.

Mhandisi na mhadhiri wa DIT, Dkt. Pius Victor Chombo, alisema mwitikio huo umeonekana wazi katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo wananchi wengi wamekuwa wakitembelea banda la taasisi hiyo kutafuta elimu kuhusu matumizi ya gesi kwenye magari.

"Watu wengi wanataka kujua wanawezaje kupunguza gharama za uendeshaji wa magari yao. Ndiyo maana mwitikio umekuwa mkubwa mwaka huu," alisema.

Matumizi ya gesi asilia yanaendelea kuwa mbadala unaovutia kwa madereva na wamiliki wa magari kutokana na gharama zake kuwa nafuu ikilinganishwa na mafuta.

Kwa mujibu wa Dkt. Chombo, DIT imekuwa ikitoa huduma za kufunga mifumo ya gesi kwenye magari pamoja na mafunzo kwa vijana wanaotaka kujifunza teknolojia hiyo.

Alisema gharama za kufunga mfumo wa gesi kwenye gari zinaanzia Tshs. Milioni 2 hadi Tdhs. 2.5 milioni, kutegemeana na aina ya mfumo unaohitajika.

"Tunawakaribisha wananchi wote wanaotaka kufunga mifumo hii pamoja na vijana wanaotaka kujifunza ili waweze kujiajiri kupitia huduma hizi," alisema.

Dkt. Chombo alisema ongezeko la matumizi ya gesi limechangia pia kuongezeka kwa karakana zinazotoa huduma za ufungaji wa mifumo hiyo nchini.

Mpaka sasa, huduma za gesi asilia zinaendelea kusambaa nje ya Dar es Salaam, huku Morogoro ikiwa miongoni mwa mikoa iliyoanza kupata miundombinu ya huduma hiyo.

Pia aliwataka vijana wa Morogoro na Dodoma kujitokeza kupata mafunzo ya ufungaji wa mifumo ya gesi ili wawe tayari kunufaika na fursa mpya zinazotokana na upanuzi wa matumizi ya nishati hiyo nchini.

"Kadiri vituo vya gesi vinavyoendelea kuongezeka, ndivyo mahitaji ya wataalamu wa kufunga mifumo hii yatakavyoongezeka," alisema.

DIT imeendelea kutumia maonesho ya Sabasaba kutoa elimu kuhusu matumizi ya gesi asilia kama sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kupunguza gharama za usafiri kwa wananchi.