Mabena: JKT inawajenga vijana kwa ujuzi wa maisha na kazi

 

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, amesema Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linaendelea kuwajengea vijana nidhamu, uzalendo na stadi za kazi zinazowawezesha kujitegemea baada ya mafunzo.

Mabena alisema hayo Julai 11, 2026 alipotembelea banda la JKT katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Alisema mbali na mafunzo ya awali ya kijeshi, vijana wanaopitia JKT hupata maarifa ya kazi na maisha yanayowasaidia katika kujiajiri na kushiriki shughuli za maendeleo.

"Vijana wetu wanajifunza nidhamu na uzalendo, lakini pia wanapata stadi za kazi ambazo zinawasaidia kujenga maisha yao baada ya mafunzo," alisema.

Mabena pia alipongeza shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa kupitia kampuni tanzu ya SUMA JKT.

Alisema bidhaa na huduma zinazotolewa na SUMA JKT zimeendelea kupata sifa kutokana na ubora wake.

"Watanzania wanazipenda sana bidhaa zetu. Rai yangu kwa SUMA JKT na vikosi vya JKT ni kuongeza uzalishaji huku ubora ukiendelea kubaki wa kiwango cha juu," alisema.

Kwa mujibu wa Mabena, ongezeko la uzalishaji litasaidia wananchi wengi zaidi kupata bidhaa za ndani huku likichangia ukuaji wa uchumi na ajira.

Katika maonesho hayo, JKT imeonyesha bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia vikosi vyake na SUMA JKT kama sehemu ya kuonesha mchango wake katika maendeleo ya taifa.