NEMC: Taka ni fursa, si tatizo

Na Charles Mkoka 

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema taka zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira, biashara na kipato endapo zitachambuliwa na kurejelewa kwa njia sahihi.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaliyofanyika sambamba na Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, alisema mazingira hayawezi kulindwa na Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wananchi, sekta binafsi, taasisi za elimu na vijana.

"Mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu. Tunahitaji ushirikiano wa wadau wote ili kulinda rasilimali zetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," alisema.

Dkt. Semesi alisema moja ya maeneo yenye fursa kubwa kwa sasa ni urejelezaji wa taka.

"Kwetu sisi NEMC, taka ni fursa. Ndani yake kuna ajira, biashara na mapato kwa vijana na makundi mbalimbali ya jamii," alisema.

Alibainisha kuwa vijana wanaendelea kuwa sehemu muhimu ya suluhisho la changamoto za mazingira kupitia ubunifu, teknolojia za kijani, urejelezaji na ujasiriamali.

Kijiji cha Mazingira kilichoandaliwa katika maonesho ya Sabasaba kimekuwa jukwaa la kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira, usimamizi wa taka, tathmini za athari za mazingira na biashara zinazozingatia mazingira.

NEMC pia imeendelea kuhimiza wawekezaji na watengenezaji wa miradi kufanya tathmini za athari za mazingira kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao.

Wadau wa mazingira wanasema ushiriki wa vijana, matumizi ya nishati safi na uwekezaji katika uchumi wa kijani ni miongoni mwa njia zitakazosaidia Tanzania kulinda mazingira huku ikifungua fursa mpya za maendeleo na ajira.