Mfumo wa Sema na BoT kurahisisha utatuzi wa malalamiko

NB: Picha hii imetengenezwa na kuundwa na akili unde kwa matumizi ya kuelekeza pekee. (illustration purposes)

 Na Charles Mkoka

Dar es Salaam. Wakati huduma za kifedha zikiendelea kuhamia zaidi kwenye mifumo ya kidijitali, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuimarisha ulinzi wa watumiaji kupitia mfumo wa Sema na BoT, unaorahisisha utoaji na ufuatiliaji wa malalamiko ya huduma za fedha.

Mfumo huo unawaruhusu wananchi kuwasilisha malalamiko yao na kufuatilia hatua za utatuzi bila kulazimika kutembelea ofisi za Benki Kuu. 

Malalamiko yanaweza kuwasilishwa kupitia tovuti, programu ya simu, namba ya bure na huduma ya chatbot.

Kwa kizazi cha sasa cha vijana, hususan Gen Z ambao hutumia simu kwa shughuli nyingi za kifedha, mfumo huo unatoa njia ya haraka ya kuripoti changamoto zinazohusisha benki, mikopo ya kidijitali, miamala ya simu na huduma nyingine za kifedha.

Vijana, wafanyabiashara wadogo, wakulima, wajasiriamali, watumishi wa umma na watumiaji wa huduma za fedha katika maeneo mbalimbali ya nchi wanaweza kupata haki zao bila gharama za kusafiri au kufuatilia kesi kwa muda mrefu.

BoT imeweka mkazo pia kwenye ujumuishi. Mwongozo wa ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha unazitaka taasisi za kifedha kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum na kuhakikisha taarifa za malalamiko zinapatikana kwa urahisi kwa makundi yote ya wananchi.

Habari hii inatafsirika kuwa ni muhimu na yenye uendelevu mwema kwa watu wa makundi maalum hadi wale wenye ulemavu na wananchi ambao mara nyingi hukutana na changamoto za kufikia huduma za kifedha au kupata msaada wanapopata matatizo ya miamala na mikopo. 

Mfumo huo unalenga kuhakikisha kila mtumiaji anapata nafasi ya kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa malalamiko yake.

Takwimu za BoT zinaonyesha kuwa mfumo huo umeongeza ufanisi katika uchakataji wa malalamiko kwa kuhakikisha kwanza taasisi za kifedha zinashughulikia changamoto za wateja kabla ya suala kufikishwa kwa msimamizi mkuu wa sekta hiyo. 

Hatua hiyo inatafsirika kupunguza migogoro isiyo ya lazima na kuongeza kasi ya utatuzi wa malalamiko yanayohitaji uamuzi wa mdhibiti.

Akizungumza katika Maonesho ya Sabasaba mwaka huu, alipootembelea kijiji cha BoT , Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuuboresha mfumo huo ili uwafikie wananchi wengi zaidi, wakiwemo wale ambao bado wanapata changamoto kutumia teknolojia za kisasa.

Kadiri Tanzania inavyoendelea kupanua matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali, Sema na BoT inaonekana kuwa moja ya zana muhimu zinazojenga imani, uwazi na uwajibikaji katika sekta ya fedha. Kwa mwananchi wa kawaida, ujumbe wake ni rahisi: ukipata changamoto ya huduma za fedha, sasa una sehemu ya kusema na kusikilizwa.