Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara huku mfumuko wa bei ukibaki katika kiwango cha takriban asilimia 4.
Tutuba alisema hali hiyo inatokana na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na mifumo ya kifedha inayotekelezwa na Benki Kuu.
Alizungumza leo Julai 10 baada ya kutembelea banda la BoT katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Alisema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza kazi za Benki Kuu na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Tutuba alisema uamuzi wa hivi karibuni wa kuweka kiwango cha riba ya Benki Kuu katika asilimia 6.25 unalenga kuongeza ukwasi kwenye sekta ya benki, kuchochea utoaji wa mikopo na kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei.
Alibainisha kuwa Tanzania imeendelea kuvutia wawekezaji licha ya changamoto za kiuchumi zinazoikabili dunia.
Kwa mujibu wake, mafanikio hayo yamechangiwa na sera thabiti za fedha, mifumo salama ya malipo na uwekezaji katika maendeleo ya wataalamu wa Benki Kuu.
Akiwa katika banda hilo, Tutuba pia alipata maelezo kuhusu mfumo wa Sema na BoT unaotumika kupokea na kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha.
Aliagiza mfumo huo uendelee kuboreshwa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, ikiwemo wale ambao wanapata changamoto kutumia mifumo ya kidijitali.
Tutuba alisema BoT imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966, ikiwemo kuimarika kwa sekta ya fedha, mifumo ya malipo na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.


