EAPP: Tanzania yashiriki majadiliano ya kuimarisha gridi za umeme

 

Na Mwandishi wetu

Addis Ababa. Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia na kufanya mazungumzo na Balozi Innocent Shiyo.

Ziara hiyo imefanyika wakati Makamba akiwa Addis Ababa kushiriki Mkutano wa 22 wa Baraza la Mawaziri la Soko la Pamoja la Nishati Mashariki mwa Afrika (EAPP).

Mkutano huo unawakutanisha viongozi wa sekta ya nishati kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki kujadili ushirikiano wa biashara ya umeme na maendeleo ya miundombinu ya nishati.

Makamba na Balozi Shiyo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia pamoja na maendeleo ya sekta ya nishati katika ukanda huo.

Katika ziara hiyo, Makamba aliambatana na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mipango, Utafiti na Uwekezaji wa TANESCO, HenryFried Byabato, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo.

Pia alifuatana na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati wanaoshiriki mkutano huo.

Mkutano wa EAPP unatarajiwa kuhitimishwa kwa kupitisha maamuzi muhimu yatakayochochea biashara ya umeme na kuimarisha uunganishaji wa gridi za taifa kati ya nchi wanachama.