Sodocare yaleta huduma za afya majumbani Dar es Salaam


 
Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Kampuni ya Solidarity Domiciliary Care (Sodocare) imeendelea kutoa huduma za afya majumbani kwa wagonjwa wanaoruhusiwa kutoka hospitalini lakini bado wanahitaji uangalizi wa kitabibu, pamoja na huduma ya uchuaji wa misuli au mwili (massage).

Mkurugenzi Mkuu wa Sodocare, Ashura Mwilima, amesema huduma hizo zinalenga kuwasaidia wagonjwa kuendelea kupata matibabu wakiwa katika mazingira ya nyumbani na karibu na familia zao.

Alisema kampuni hiyo huhudumia wagonjwa wenye magonjwa ya muda mrefu kama saratani, kisukari, shinikizo la damu, kiharusi na wengine.

Pia hutoa huduma za kitaalamu kama kubadilisha bandeji za vidonda, huduma baada ya upasuaji, pamoja na usimamizi wa vifaa vya kulishia na kusaidia wagonjwa wenye mahitaji maalumu.

Kwa mujibu wa Mwilima, huduma huanza baada ya timu ya wauguzi kufanya tathmini ya mgonjwa nyumbani ili kubaini kiwango cha huduma kinachohitajika.

Alisema huduma za afya majumbani huwapa wagonjwa faraja zaidi kwa kuwa karibu na familia zao huku zikipunguza gharama zinazoweza kutokea kwa kukaa hospitalini kwa muda mrefu.

"Tunaamini mgonjwa anapokuwa karibu na familia yake hupata utulivu wa akili na nguvu ya kuendelea na matibabu," alisema.

Mwilima alisema Sodocare inatumia wauguzi wenye ujuzi wa hali ya juu na vifaa vya kisasa vinavyokubalika kimataifa ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma salama na zenye ubora.


Aliongeza kuwa kampuni hiyo pia hukusanya maoni kutoka kwa wagonjwa na familia zao ili kuendelea kuboresha huduma na kuhakikisha viwango vya ubora vinaimarishwa kila wakati.

Kwa sasa, huduma za Sodocare zinapatikana katika Mkoa wa Dar es Salaam wilaya zote huku ikiendelea kuwafikia wananchi wanaohitaji huduma za afya katika mazingira ya nyumbani.