Youth4Nature yaibua kizazi kipya cha viongozi wa uhifadhi


Na Mwandishi wetu

Zaidi ya vijana 300 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekutana katika Mkutano wa Tatu wa Youth4Nature Conference 2026 uliolenga kuwajengea uwezo na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira na rasilimali asili.

Mkutano huo uliofanyika Juni 13 na 14, 2026 uliwakutanisha vijana pamoja na wadau wa uhifadhi wakiwemo wataalamu wa mazingira, watafiti, wabunifu wa teknolojia, watunga sera, wajasiriamali na viongozi wa mashirika mbalimbali.

Washiriki walipata fursa ya kujifunza namna taaluma na vipaji vyao vinavyoweza kutumika katika kutatua changamoto za mazingira. Mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo ulinzi wa bioanuwai, matumizi ya teknolojia katika uhifadhi na ushirikishwaji wa jamii katika kulinda mazingira.

Meneja wa Mkutano wa Youth4Nature 2026, Allen Chad Mgaza, amesema mwitikio mkubwa wa wataalamu kushiriki mkutano huo ni ishara kuwa sekta ya uhifadhi imeanza kutambua mchango wa vijana katika kuleta mabadiliko.

Amesema waandaaji walipokea zaidi ya maombi 130 kutoka kwa watu waliotaka kuwa wazungumzaji, huku wengi wao wakiwa wataalamu waliokuwa tayari kushirikisha maarifa na uzoefu wao kwa kizazi kipya cha wahifadhi.

Kwa mujibu wa Allen, takribani asilimia 70 ya waombaji hao walikuwa vijana wanaofanya kazi katika sekta ya uhifadhi. Hali hiyo inaonyesha kuwa vijana sasa si watazamaji, bali ni sehemu ya viongozi wanaoshiriki kufanya tafiti, kuendesha miradi na kuibua suluhisho za changamoto za mazingira.

Mkutano huo pia uliangazia nafasi ya teknolojia katika uhifadhi. Mtaalamu wa teknolojia, Francis Mhalafu, alisema matumizi ya Akili Bandia (AI) yanaweza kusaidia kuboresha ufuatiliaji wa wanyamapori, uchambuzi wa taarifa za mazingira na utoaji wa elimu kwa jamii.

Alisema dunia ya sasa inahitaji ushirikiano wa taaluma mbalimbali katika kulinda mazingira. Kwa hiyo vijana wenye ujuzi wa teknolojia, sayansi ya data, uhandisi na mawasiliano wana nafasi kubwa ya kutoa mchango katika sekta ya uhifadhi.

Allen alisema uzoefu wake katika masuala ya uhifadhi umeonyesha kuwa vijana wana hamasa kubwa ya kushiriki katika kulinda mazingira, lakini wanahitaji kupewa maarifa, ushauri wa kitaaluma na fursa za kujifunza kutoka kwa wataalamu waliobobea.

Mkutano wa Youth4Nature 2026 umeonyesha kuwa Tanzania ina kundi kubwa la vijana wenye uwezo wa kutumia sayansi, teknolojia, ubunifu na ushirikiano wa kijamii kuendeleza juhudi za uhifadhi. Waandaaji wanaamini uwekezaji kwa vijana wa leo ni msingi wa mafanikio ya uhifadhi wa kesho.