Baadhi ya wananchi waliotembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) wamewahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo, wakisema hali ya usalama ndani na nje ya viwanja hivyo ni nzuri na inawapa wageni fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali kwa utulivu.
Mohammed Omari Tego, mkazi wa Mbagala, alisema amefika katika viwanja vya Sabasaba na kushuhudia mazingira ya amani tangu alipoingia hadi muda wa kuondoka.
“Mpaka sasa sijakutana na vurugu wala usumbufu wa aina yoyote. Nimekuta amani na watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida,” alisema.
Alisema maonesho hayo yanatoa huduma nyingi muhimu katika eneo moja, jambo linalorahisisha wananchi kupata huduma wanazohitaji.
“Kuna mabanda mengi yenye huduma mbalimbali. Ukihitaji huduma za NIDA, benki na taasisi nyingine, unazipata hapa kwa urahisi. Nawashauri wananchi walio nyumbani wajitokeze kutembelea maonesho haya,” alisema.
Kwa upande wake, Ahmad Ali Ndomondo kutoka Mbagala, mtaa wa Kingugi, alisema alifika Sabasaba kwa lengo la kupata huduma ya kupima macho na kujionea hali halisi ya maonesho hayo.
Alisema kabla ya kufika alipokea taarifa kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa na wasiwasi kuhusu hali ya usalama, lakini baada ya kuingia ndani ya viwanja alikuta mazingira salama na tulivu.
“Nilipofika hapa nimekuta hali ni shwari. Mabanda yote yanaendelea kutoa huduma vizuri na wageni wanapokelewa kwa heshima. Hakuna sababu ya kuwa na hofu,” alisema.
Ndomondo aliongeza kuwa uwepo wa vyombo vya ulinzi na usalama umeendelea kuwapa wananchi uhakika wa usalama wao na mali zao wanapokuwa viwanjani hapo.
Aliwataka wananchi kutumia siku zilizobaki za maonesho hayo kutembelea mabanda mbalimbali, kujifunza kuhusu bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi za umma pamoja na sekta binafsi.
Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuvutia maelfu ya wageni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanaofika kujionea maendeleo ya biashara, uwekezaji, teknolojia na huduma zinazotolewa na washiriki wa maonesho hayo.