Morogoro — Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB imeboresha Hatifungani ya Miundombinu ya Barabara za Wilaya (Samia Infrastructure Bond) ili kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa makandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara nchini.
Hatua hiyo inalenga kusaidia makandarasi kupata mtaji kwa wakati, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuhakikisha barabara zinazojengwa chini ya usimamizi wa TARURA zinakamilika kwa muda uliopangwa.
Akizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wahasibu wa TARURA, wataalamu wa Benki ya CRDB, mameneja wa mikoa na makandarasi, Mhasibu Mkuu wa TARURA, CPA Jacob Nyaulingo, alisema maboresho hayo yataongeza uwezo wa makandarasi kupata fedha za kuendesha miradi yao kwa urahisi zaidi.
“Hatifungani hii imeboreshwa na tunawahimiza makandarasi nchini kuitumia ili kupata fedha za kutekeleza miradi kwa wakati na kwa ufanisi,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Mikopo wa Benki ya CRDB, Michael Paul, alisema serikali imefanya maboresho ya taratibu za upatikanaji wa mikopo kupitia mpango huo, jambo ambalo limeongeza urahisi kwa makandarasi kupata fedha za kuendesha shughuli zao.
Alisema lengo la ushirikiano huo ni kuhakikisha changamoto ya mtaji haikwamishi utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na TARURA.
Mmoja wa wanufaika wa mpango huo kutoka kampuni ya MORCEP, Nasra Ramadhani, alisema kampuni yake imekuwa ikitumia mikopo inayotolewa kupitia Samia Infrastructure Bond kutekeleza miradi mbalimbali kwa wakati.
Alisema upatikanaji wa fedha umekuwa rahisi na umesaidia kampuni kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa kazi za ujenzi wa miundombinu.
Mpango wa Samia Infrastructure Bond ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha utekelezaji wa miradi ya barabara za vijijini na mijini kwa kuwezesha makandarasi kupata mitaji ya uhakika kwa ajili ya kazi za maendeleo.