MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA YAANDAA CITY TOUR YA KIHISTORIA, WADAU WAJIFUNZA URITHI WA TAIFA

Makumbusho ya Taifa la Tanzania leo imefanikisha City Tour maalum iliyowaleta pamoja wadau mbalimbali wa utalii katika safari ya kujifunza historia, utamaduni na urithi wa Tanzania kupitia maeneo muhimu ya kihistoria na kitamaduni yaliyopo jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo imeanza katika Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo washiriki walipata utambulisho wa safari hiyo kabla ya kuanza kutembelea maeneo mbalimbali ya urithi.

Baada ya hapo, msafara ulielekea Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, ambako washiriki walipata fursa ya kujifunza historia ya binadamu tangu enzi za kale, maendeleo ya jamii za Kitanzania na urithi wa taifa unaohifadhiwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. Washiriki wakitembelea maonesho mbalimbali, walipata maelezo kutoka kwa mtaalamu wa Makumbusho na kisha kupata fursa ya kuuliza maswali yaliyoongeza uelewa wao kuhusu historia ya Tanzania.

Safari iliendelea katika Kijiji cha Makumbusho, ambako wadau walijionea nyumba za asili za makabila mbalimbali ya Tanzania, mila na desturi zinazodhihirisha upekee wa utamaduni wa Mtanzania. 

Aidha, wamepata nafasi ya kuzunguka na kujifunza historia ya Mbuyu maarufu, ambao ni sehemu ya urithi unaobeba simulizi za kihistoria na kitamaduni.

Ziara hiyo imehitimishwa katika eneo la TAWA Kunduchi Ruins, ambapo washiriki wametembelea mabaki ya kihistoria yanayodhihirisha ustaarabu wa zamani wa mwambao wa Afrika Mashariki. Wataalamu wametoa maelezo ya kina kuhusu historia ya eneo hilo na umuhimu wake katika kuhifadhi urithi wa taifa.

City Tour hiyo imeonyesha dhamira ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania ya kuendelea kuelimisha umma, kutangaza vivutio vya urithi wa utamaduni na historia, pamoja na kuhamasisha Watanzania na wageni kutembelea maeneo ya urithi kama sehemu ya kukuza utalii wa utamaduni nchini.

Makumbusho ya Taifa la Tanzania inanaendelea kutumia fursa mbalimbali za maonesho na programu za elimu kuwafikia wananchi na wadau, kwa lengo la kuhakikisha urithi wa taifa unafahamika, unathaminiwa na unaendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

soma