Na Mwandishi wetu
Geita. Serikali imesema wakati umefika kwa vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 kutoa ushuhuda wa mafanikio yaliyopatikana kupitia fedha hizo badala ya kuendelea kueleza changamoto za utekelezaji wa mpango huo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, wakati akizindua Kikundi cha Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu cha AMANI katika Kata ya Bukoli, Jimbo la Busanda mkoani Geita.
"Hatuhitaji kuendelea kusikia changamoto. Tunataka kusikia ushuhuda wa waliopokea mikopo na kufanikiwa ili wawe mfano kwa wengine," alisema Dkt. Seif.
Alisema kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuridhia utolewaji wa mikopo hiyo ilikuwa kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupata mitaji ya kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Dkt. Seif, sasa ni wakati wa kuona mikopo hiyo ikizalisha matokeo yanayoonekana kupitia ongezeko la kipato, ajira na maendeleo ya wanufaika.
Uzinduzi wa kikundi hicho uliambatana na harambee ya kuchangisha Sh200 milioni kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya kisasa ya kukoboa mpunga na ujenzi wa ghala la kuhifadhi zaidi ya magunia 20,000 ya mazao.
Dkt. Seif alichangia kufanikisha upatikanaji wa zaidi ya Sh38 milioni kupitia michango ya fedha taslimu na ahadi kutoka kwa viongozi, wananchi, madiwani na wadau mbalimbali.
Pia aliwataka Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kuendelea kufuatilia na kuvilea vikundi vinavyonufaika na mikopo hiyo ili viweze kukua na kuleta manufaa kwa wanachama wake.
Kikundi cha AMANI kina wanachama 90 na kimekuwa kikijishughulisha na shughuli za kiuchumi kwa zaidi ya miaka miwili.


