Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Wasanii mbalimbali nchini wamejiunga na kampeni za kuhamasisha utunzaji wa mazingira kupitia uteuzi wao kama mabalozi wa mazingira, wakisimamiwa na NEMC.
Hatua hiyo ilitangazwa katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo wasanii Mycoely Mrisho Mpoto na Mzee Yusuf walitambulishwa mbele ya wananchi na wadau wa mazingira.
Pia, msanii Frida Amani alitambuliwa kuwa sehemu ya mabalozi wa mazingira, licha ya kutokuwepo katika hafla hiyo kutokana na sababu zilizomzuia kuhudhuria.
NEMC, ambao ndio waandaaji wa kampeni hiyo walisema kuwa mabalozi hao watashiriki kwa mwaka mzima kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira.
Lengo ni kutumia ushawishi wa wasanii kufikisha ujumbe wa utunzaji wa mazingira kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Katika hafla hiyo, washindi wa shindano la Mazingira Challenge pia walitambuliwa na kutunukiwa zawadi kwa mchango wao katika kuhamasisha masuala ya mazingira.
Wadau wa mazingira wanaamini ushiriki wa wasanii utaongeza mwamko wa wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi na usimamizi bora wa mazingira.
Kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali na kujenga jamii inayojali mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.

