JAB yazindua ithibati ya maisha kwa waandishi wa habari wakongwe

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezindua rasmi Mwongozo wa Kisheria wa Utoaji wa Ithibati ya Maisha kwa Waandishi wa Habari Wakongwe.

Hatua hiyo inalenga kutambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari waliolitumikia taifa kwa muda mrefu na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tasnia ya habari nchini.

Uzinduzi huo umefanyika Julai 11, 2026 wakati wa maadhimisho ya JAB Day katika Banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Kupitia hotuba iliyosomwa na Dkt. Egbert Mkoko, Mwenyekiti wa JAB, Tido Mhando, alisema mwongozo huo umeandaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ili kuweka utaratibu maalumu wa utoaji wa ithibati ya maisha kwa waandishi wa habari wakongwe.

Alisema mwongozo huo unawahusu waandishi ambao mwaka 2016 walikuwa na umri wa miaka 50 au zaidi na walikuwa tayari wametoa mchango mkubwa katika taaluma ya habari.

"Mwongozo huu unalenga kuhifadhi historia ya tasnia ya habari na kuthamini mchango wa waandishi wa habari wakongwe," ilieleza sehemu ya hotuba hiyo.

Mhando alisisitiza kuwa mwongozo huo hauondoi masharti ya msingi yaliyowekwa na sheria kuhusu utoaji wa ithibati kwa waandishi wa habari.

Badala yake, alisema unaweka utaratibu wa kutekeleza mamlaka ya Bodi ya kutoa ithibati ya maisha kwa waandishi waliotoa mchango wa kipekee katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Bodi ya kuimarisha taaluma ya habari huku ikitambua mchango wa waandishi wakongwe.

"Tunataka kuendeleza viwango vya taaluma lakini pia kuthamini wale waliolitumikia taifa kwa uaminifu, uzalendo na weledi," alisema.

Sambamba na uzinduzi huo, wadau wa sekta ya habari walikutana katika mdahalo maalumu kujadili maendeleo ya tasnia, utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari na uzoefu wa mwaka mmoja wa mfumo wa utoaji wa ithibati kwa waandishi wa habari.