Na Mwandishi wetu
Kagera. Serikali imefanikiwa kukamata dhahabu yenye thamani ya zaidi ya TShs. Bilioni 1.3 iliyokuwa ikitoroshwa kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria.
Dhahabu hiyo ilikamatwa kupitia operesheni iliyofanyika Julai 1, 2026 kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi, Tume ya Madini, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Kikosi Kazi cha Kuzuia Utoroshaji wa Madini.
Akizungumza Julai 13 mkoani Kagera, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, alisema madini yaliyokamatwa ni vipande 163 vya dhahabu vyenye uzito wa gramu 4,434.66.
Baada ya tathmini kufanyika, thamani ya dhahabu hiyo ilifikia Sh1.345 bilioni.
"Serikali imejipanga kuhakikisha rasilimali za madini zinalindwa na kunufaisha Watanzania kupitia mifumo rasmi ya biashara," alisema Dkt. Kiruswa.
Alitoa onyo kwa watu na mitandao inayojihusisha na biashara haramu ya madini, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Kwa mujibu wa Dkt. Kiruswa, kati ya Julai 2025 na Machi 2026, Serikali imefanikiwa kukamata madini yenye thamani ya Sh3.31 bilioni katika matukio 55 yaliyorekodiwa sehemu mbalimbali nchini.
Alisema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti utoroshaji wa madini.
Dkt. Kiruswa aliwataka wachimbaji, mawakala wa madini, wafanyabiashara na wananchi kutumia masoko rasmi ya madini pamoja na vituo vya ununuzi vilivyoanzishwa nchini kufanya biashara zao kwa usalama na kwa mujibu wa sheria.
"Tunayo zaidi ya masoko 40 ya madini nchini. Tunawahimiza wadau wote kutumia mifumo rasmi ili kulinda biashara zao na kuongeza mchango wa sekta hii katika uchumi wa taifa," alisema.


