DMI yatumia Sabasaba kuhamasisha udahili wa mwaka 2026/27

 

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Taasisi ya Bahari Dar es Salaam (DMI) imeanza kampeni ya kuhamasisha udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2026/27 kupitia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Mkufunzi Msaidizi wa DMI, Wilfrida Wenceslaus Ngallu, alisema taasisi hiyo inaendelea kupokea maombi ya wanafunzi wanaotaka kujiunga na programu mbalimbali za bahari.

Alisema udahili unahusisha kozi za cheti, diploma, shahada, shahada za uzamili pamoja na kozi za umahiri wa mabaharia.

Kwa mujibu wa Ngallu, dirisha la kwanza la udahili kwa kozi za cheti, diploma, shahada ya uzamili na umahiri wa mabaharia litafungwa Julai 11.

Aliongeza kuwa maombi ya kozi za shahada yanatarajiwa kuanza Julai 15.

Ngallu alisema DMI inatoa mafunzo yanayotambuliwa kitaifa na kimataifa, yakilenga kuzalisha wataalamu wa sekta ya bahari wanaohitajika ndani na nje ya nchi.

Pia aliwahamasisha wasichana na wanawake kujiunga na taaluma za bahari, akisema sekta hiyo ina fursa nyingi zinazoweza kufikiwa na kila mtu.

"Wasichana wana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika taaluma hizi. Tunahitaji kuona wanawake wengi zaidi wakichangamkia fursa zilizopo katika sekta ya bahari," alisema.

Kwa upande wa sifa za kujiunga, waombaji wa kozi za cheti wanapaswa kuwa na angalau ufaulu wa alama D nne katika mtihani wa kidato cha nne.

Kwa diploma, mwombaji anatakiwa kuwa na angalau ufaulu wa E au S katika kidato cha sita au cheti husika.

Waombaji wa shahada wanapaswa kuwa na principal passes mbili za kiwango cha D katika kidato cha sita au diploma yenye GPA ya angalau 3.0.

Kwa shahada ya uzamili, mwombaji anatakiwa kuwa na shahada ya kwanza yenye GPA ya angalau 2.7.

DMI imewataka wanafunzi na wazazi kutembelea banda la taasisi hiyo Sabasaba au kuwasilisha maombi kupitia mfumo wa udahili wa mtandao.