Turkys Group yatumia Sabasaba kuonyesha uwekezaji wake Tanzania

 


Na Charles Mkoka

Dar es Salaam. Turkys Group of Companies imetumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuonyesha bidhaa, huduma na miradi yake mbalimbali inayotekelezwa nchini.

Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni hiyo, Juma Mnaro, amesema maonesho hayo ni fursa muhimu ya kukutana na wateja, washirika wa biashara na wawekezaji.

Kupitia kampuni yake tanzu ya Zen General Merchandise, Turkys Group inaonyesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini. Miongoni mwao ni mafuta ya kupikia, sabuni za matumizi ya nyumbani na mchele.

Katika Sabasaba ya mwaka huu, kampuni hiyo pia imezindua aina mbili mpya za sabuni zenye harufu ya lavender na limao.

Mbali na bidhaa za matumizi ya kila siku, Turkys Group inaendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, usafirishaji, maghala ya kisasa, ujenzi wa majengo, uzalishaji wa saruji na huduma za uhandisi.

Kampuni hiyo pia imeonyesha maji ya kunywa yaliyowekwa kwenye chupa za kioo pamoja na mifuko maalumu inayoweza kutumika mara nyingi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda mazingira.

Mnaro alisema Turkys Group ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha huduma za kubadilisha magari kutumia gesi asilia (CNG), hatua inayolenga kupunguza gharama za mafuta na kusaidia matumizi ya nishati safi.

Aidha, kampuni hiyo imeonyesha uwekezaji wake katika sekta ya afya kupitia hospitali zinazotoa huduma Zanzibar na Dar es Salaam.

Aliwahamasisha wananchi kutembelea banda la Turkys Group ili kujifunza zaidi kuhusu bidhaa, huduma na fursa za uwekezaji zinazotolewa na kampuni hiyo.