Na Mwandishi wetu
Dodoma. Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kukatika kwa umeme kwa muda katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro na Tanga kuanzia Julai 9 hadi Julai 14, 2026 ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya umeme.
Hatua hiyo inalenga kupisha kazi za ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo, huduma ya umeme itasitishwa kwa siku husika kuanzia saa 1:00 usiku hadi saa 12:00 jioni.
TANESCO imesema kazi zinazofanyika ni pamoja na uwekaji wa nyaya katika mradi huo mkubwa wa gridi ya taifa.
Maeneo yatakayoathirika ni pamoja na Mkulazi, Turiani, Mvomero, Kilosa, Kilindi na Gairo.
Baadhi ya taasisi za Serikali, makazi ya wananchi, maeneo ya kilimo na vituo vya huduma za kijamii pia vitaathirika katika kipindi hicho.
Shirika hilo limesema usitishaji wa huduma ni wa muda na unalenga kuhakikisha kazi zinafanyika kwa usalama na kwa wakati.
TANESCO imewaomba wananchi kuwa na uvumilivu huku ikiwataka kuepuka kugusa nyaya za umeme zilizoanguka au kuning'inia chini.
Wananchi wametakiwa kutoa taarifa za dharura kupitia namba ya huduma kwa wateja 180 pindi changamoto yoyote Ile itakapojitokeza.
